Ufaransa ilishinda kwa mbinde mchezo wake kwanza dhidi ya Romania, shukrani za dhati ziende kwake Dimitri Payet ambaye alifunga goli la ushindi dakika za majeruhi baada ya kuhamishiwa namba 10, kufuatia kutolewa kwa Paul Pogba na nafasi yake kuchukuliwa na Anthony Martial, ambaye alienda pembeni alipokuwa akicheza Payet.
Hakuna matarajio yoyote ya Deschamps kufanya mabadiliko katika kikosi kilichoanza siku ya ufunguzi, lakini kiwango bora cha Payet kinaweza kumshawishi kufanya mabadiliko ya namba endapo Pogba hataonesha kiwango cha kuridhisha kwa mara nyingine leo.
Antoine Griezmann pia hakuwa katika ubora wake, lakini ni matarajio yangu kwamba ataanza katika nafasi yake dhidi ya kinda Kinsley Coman, huku Giroud pia akiendelea kubaki kama mtu wa mwisho kutokana na ubora wake anaoendelea kuonesha mbele ya lango.
Albania kwa upande wao, wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Uswizi na bado wanabaki na matumaini ya kusonga mbele endapo tu watashinda mchezo wa leo.
Licha ya kucheza pungufu kwa takriban dakika 54 baada ya nahodha wao Loric Cana kutolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini Albania walionesha kiwango cha hali juu sana. Walikuwa na bahati mbaya kutopata bao la kusawazisha katika dakika za mwisho baada ya kipa wa Uswizi kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari nyingi ambazo zingeleta madhara makubwa.
Lakini katika mchezo wa leo, Ufaransa wanapewa nafasi kubwa zaidi, lakini hofu yao kubwa inakuja kutokana na kutokuwa na rekodi nzuri dhidi ya wapinzani wao katika michezo miwili iliyopita.

No comments:
Post a Comment